Malaki 3:1-12
Ule mstari wa nne na wa tano
unasema “wakati
ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zintakapopendeza mbele za Bwana, kama
katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani nami nitawakaribieni ili
kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu wa wazinzi, na
juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa
ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate
haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi”
Mpenzi msomaji sijui kama
unajua kwamba neno la Mungu ni jumla ya mawazo na majibu ya Mungu kwa
mwanadamu. Kuna siri nyingi sana ndani ya Biblia, ambazo si rahisi kuzielewa
mpaka Roho wa Yesu akufunulie kwa utukufu wake utakapomtafuta.
Ilikuwa tarehe 31/08/2008,
wakati naomba nilimuuliza Mungu maswali mawili ya kifedha. Moja lilihusu
ujenzi wa kanisa la mahali ninapoabudu na la pili lilihusu mahitaji yangu ya
kifedha. Baada ya maombi hayo ndipo Mungu aliponifunulia siri hii nami
nataka nikushirikishe. Ukiweka kwenye matendo siri hii naamini maisha yako ya
kiuchumi yatabadilika na kuwa bora zaidi.
Inawezekana maisha yako
kiuchumi kwa sasa si mazuri, biashara zako pia hazijakaa vema, miradi yako pia
haijakaa vema ni kama haisongi mbele, kuomba unaomba, yumkini na fungu la kumi
unajitahidi kutoa, na sehemu ya mapato yako unapeleka kwa watumishi, bado kuna
fungu jingine hata maskini unawasaidia.
Huenda pia kama ni mwajiriwa
selikarini au taasisi binafsi n.k unaona hautendewi haki katika malipo
mbalimbali na hata mshahara wako pia. Huenda wewe ni yatima au mjane
halafu kuna haki zako ambazo zimetekwa na yule adui, huenda ni sehemu ya
mirathi yenu, huenda kama wewe ni mjane basi stahili na mali ulizotafuta na
mume wako zimechukuliwa na maisha ni magumu, unaona kama Mungu amekusahau na
umeenda kwenye vyombo vya sheria lakini ufumbuzi bado haujapatikana nk.
Leo nina habari njema kwako,
usidhani Mungu amekusahau, isipokuwa wewe ndio umemsahau, “Naam umemsahau”.
Mungu anachotaka ni kukupigania katika haki zako. Mungu hafurahii
unayoyapitia anataka upate haki zako zote. Sasa ili uweze kupata haki
zako ni lazima ujifunze
na uanze kutoa dhabihu/sadaka za haki na za kumpendeza yeye.
Yawezekana pia baraka/haki
zako zimetekwa na wachawi, wazinzi, na watu waapao kwa uongo na wenye
kukuonea. Wewe huna uwezo wa kuwashinda hawa watu kwa nguvu zako, naam Mungu anao uwezo
huo. Nguvu
za Mungu za kukupigania na kurejesha baraka/haki zako zimo katika wewe kutoa
sadaka za haki na za kumpendeza yeye. i.e Kadri unavyotoa sadaka
za haki ndivyo unavyomkaribisha Mungu kukupigania na mbili ndivyo
unavyowasogeza adui zako mbele za Mungu awashughulikie. Unamfanya Mungu
asistarehe juu ya adui zako.
Mungu anposema wachawi
uwe na hakika anazungumzia watu ambao wanalenga kuharibu uchumi na mafanikio
yako kwa ujumla katika kila nyanja biashara,kikazi,kilimo,
kiroho,kihuduma nk, na anaposema wazinzi
ana maana mbili moja ni hawa wazinzi/ makahaba wa kawaida ambao yumkini
unatafuta fedha yako kwa jitihada lakini inaishia kwa hao na pili ni wale
waganga wa kienyeji na watumishi/manabii wa uongo, wanaosema Bwana amesema toa
hiki na kile utabarikiwa, huku mioyoni mwao wakijua hayo ni mawazo yao na si
Bwana.
Kibiblia huu ni uzinifu
wa rohoni. Yaani wamezini katika roho zao kwa kujifanya wana
nena neno la Bwana kumbe ni mawazo yao.
Na anaposema waapao kwa uongo
maana yake anazungumzia waongo kwa ujumla wanaweza kuwa washirika wako
kibiashara, kikazi, kihuduma n.k watu wanaotumia uongo kukuibia pesa yako, muda
wako, maendeleo yako wanaokopa wasilipe n.k Je kwa nini hayo yote yanakukuta wewe?
. Ni kwa sababu bado
hujatoa dhabihu za haki na za kumpendeza Mungu, naam bado hujatoa.
Je, Kutoa dhabihu za haki na
za kumpendeza Mungu ndio kukoje?
Ni kutoa kwa muda na uongozi
wa Mungu matoleo yako mbalimbali. Si watu wengi wenye
nidhamu hii. Pesa na utajiri ambao Mungu anakupa mkononi mwako ni kwa ajili ya
kuimarisha agano lake pia. Yaani kuhakikisha makusudi yake hapa duniani
yanafanikiwa kwa kutumia watu anaowabariki. Kumbuka kufanikiwa kwa makusudi ya
Mungu duniani kunategemea utiifu wa watu wake duniani.
Sasa
hii ni pamoja na wewe kama mtu wa Mungu kutoa fedha yako kwa ajili kazi ya
Mungu hapa duniani.
Suala sio kutoa tu, bali ni
kutoa kwa kufuata muongozo wa Roho Mtakatifu ndani yako kwa maana ya wapi
upeleke sadaka yako na pili kutoa kwa muda unaotakiwa kutoa kwa maana ya
lini/wakati gani unatakiwa kutoa.
Jambo hili linaweza kuonekana
gumu kwa jinsi ya kibinadamu, lakini huku ndiko kuongozwa na Roho Mtakatifu
katika utoaji.
Kama
ukiweka mahusiano yako na Roho Mtakatifu kuwa mazuri ni rahisi sana kuona
uongozi wake juu ya matoleo yako. Fahamu kwamba baraka za
mtaoaji zimefungwa
katika muda na eneo/mahali anapotoa. Hii ina maana kila
sadaka unayotoa ina baraka zake. Sasa baraka hizo zinategemeana na namna
unavyotoa kwa maana ya muda na eneo.
Kwa hiyo jifunze kutoa kwa
uongozi wa Mungu, kabla hujatoa sadaka yako, jifunze kumuuliza Mungu je sadaka
hii napeleka wapi na kwa muda gani? Kwa kufanya hivyo utakuwa
umetengeneza mazingira ya Mungu kufungua baraza zako kifedha/kiuchumi n.k.
Kama huoni baraka za Mungu kifedha kwako huenda ni kwa sababu umezizuia
kwa kutotoa dhabihu (sadaka) za haki na za kumpendeza Mungu. Neno kumpendeza Mungu
linawakilisha kiasi/kiwango na muda. Maana yake toa kwa kiwango anachotaka yeye
kwa ajili ya kazi yake na si kwa kiwango unachotaka wewe na pili toa kwa muda
anaotaka yeye na si wewe. Kinachosisitizwa
hapa pia ni uaminifu katika kutoa na si kumuibia Mungu
(Malaki 3:8).
Na Patrick Sanga
No comments:
Post a Comment