Waziri wa Mambo ya ndani Mh Dr Emmanuel Nchimbi |
Umoja
wa Wachungaji wa Makanisa ya Mkoa wa Tanga umesema hauridhishwi na taarifa
zinazotolewa na serikali na viongozi wa siasa kuwa wanaohusika na uchomaji wa
makanisa ni wahuni na si Waislamu wakati wanazuoni na masheikh wa taasisi
za kiislamu wanakiri vitendo hivyo vinafanywa na baadhi ya waumini wenzao.
Umoja
huo umesema unashangazwa na kitendo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk.
Emmanuel Nchimbi ambaye naye anavihusisha vitendo hivyo kufanywa na wahuni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa umoja huo, Dk. Jonathan
Mwakimage, alisema serikali inapaswa kushughulikia kiini cha matatizo
yanayopelekea kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwachukulia hatua
kali za kisheria wanaowashawishi vijana kufanya vitendo vya kihalifu.
Alisema
hawajaridhishwa na namna ambayo serikali imekuwa ikishughulikia wahusika wa
vitendo hivyo huku baadhi wakiendelea kuwa na kiburi na kujiona kuwa wako juu
ya sheria.
Alisema
kumeibuka kundi la watu ambao wamekuwa wakiwashawishi vijana kufanya vitendo
vya kuhujumu vitabu vitakatifu jambo ambalo limekuwa likichukuliwa na serikali
kama kitu cha kawaida.
“Hapa
Tanga kuna makanisa manne yamechomwa moto na taarifa zilifika polisi lakini
hakuna hatua zilizochukuliwa, kuna biblia zilichanwa na kukojolewa mwezi
uliopita lakini bado kimya na wahusika wanaendelea kujinadi tu mitaani, sisi
haturidhishwi na namna ambayo serikali inachukua hatua,” alisema Askofu huyo.Alisema
kuwa umoja huo wa makanisa unalaani vikali kitendo cha kukojolewa kwa Qurani,
lakini pia unaona kuwa yule aliyemshawishi mwenzake kufanya kitendo hicho ni
mkosaji wa kwanza na anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria sawa na huyo
aliyetekeleza kitendo hicho.
Hata
hivyo, aliwaomba maaskofu na wachungaji kuendelea kuwa wavumilivu katika
kipindi hiki kwa kuepuka kulipa kisasi na kuwasihi waumini wao hususan vijana
kujiepusha na waovu wanaowashawishi kukojolea, kuchoma au kuchana Quran.
“Katika
hili niwaombe Mashehe, Maimam na viongozi wa kiroho wa dini ya Kiislamu kuwa na
msimamo mkali kushughulikia waumini wao kwa kukemea vitendo hivyo kwa wazi ili
kudhibiti wenye nia ovu…hii ni pamoja na misikiti inayoendelea kuchochea chuki
dhidi ya ukristo na serikali na hasa suala la uchomaji wa makanisa” alisema Dk.
Mwakimage.
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Canon James Dominic, wa Kanisa la
Anglikana, aliitaka jamii kutambua kuwa watu wote wana asili ya tumbo moja
kutoka kwa Hawa na Adamu na kwa kutambua hilo Watanzania wanapaswa kuishi kwa
umoja, utulivu, amani na upendo.
Alisema
ni vigumu kuamini kuwa mtu mwenye dini ya kweli na kumwamini Mwenyezi Mungu kwa
dhati anaweza kufanya vitendo hivyo na hasa kwa kutambua kuwa vita ya kidini
haina mshindi na ni sumu mbaya kwa usalama wa Taifa.
Umoja
huo unahusisha makanisa yote yaliyopo mkoani Tanga kasoro la Roman
Catholic na la Sabato.
No comments:
Post a Comment