Biblia imeshaweka wazi katika Yerema 29:11 na 3 yohana 1:2 kwamba
mawazo aliyonayo Mungu juu yetu ni mawazo/mipango ya kutufanikisha, si hivyo tu
bali anataka tufanikiwe katika mambo yote. Pia tunajua kwamba fedha na dhahabu
ni mali ya Bwana si hivyo tu bali sehemu kubwa ya Biblia imejaa ahadi za Mungu
za kutufanikisha kifedha na mafundisho mengi ya pesa.
Sasa licha ya haya yote na ukweli kwamba
tumemwamini huyu Yesu lakini bado maisha ya mkristo mmoja mmoja, wakristo
wengi, kanisa kwa ujumla, kwaya, makundi ya kiroho na huduma mbalimbali hali
yake ya kifedha ni ngumu. Kila mtu analalamika juu ya pesa, mpaka imefika
mahali tatizo la fedha limekuwa sehemu ya maisha.
Mikutano, semina tumeshindwa kufanya
kisa fedha, vijana wameshindwa kuoa kisa pesa, kwaya hazirekodi kisa fedha.
Kitu gani kimetokea kwa wakristo. Wazungu wanasema “Something must be wrong
some where” maana yake lazima kuna kitu hakijakaa sawasawa mahali fulani.
Kusudi la waraka huu mfupi ni
kukuelezea sababu ambazo zimepelekea tatizo la fedha kuwa sugu na kwa sehemu ya
maisha kwa wakristo wengi. Sababu hizo ni ;
Moja,
kukosa maarifa (mafundisho) ya kutumia fedha ki-Mungu.
Hosea 4:6a Fedha ina kanuni zake za matumizi. Hivyo kushindwa kujua
kanuni hizo na namna ya kuzitumia hizo fedha ki-mungu basi tatizo litaendelea
kuwapo.
Mbili,
matumizi ya fedha ya Mungu nje ya kusudi lake.
Hagai 2:8, Sikiliza fedha ni mali ya
Bwana, hata ikiwa mikononi mwako bado ni ya Bwana, hivyo ni lazima itumike kwa
mapenzi yake, maana kila pesa anayokupa ndani ina kusudi fulani au anakupa kwa
lengo fulani.
Tatu,
Roho ya mpinga kristo inafanya kazi ndani ya fedha.
2 wathesalonike 2:7, sikiliza, shetani anajua ukiwa na fedha yeye atakuwa
na hali ngumu sana maana utaituma hiyo fedha kuimarisha agano la Bwana, hivyo
ameweka Roho ya mpinga kristo ndani ya fedha ila kupinga fedha isiende
kwa watu wa Mungu ili washindwe kumtumikia Mungu.
Nne,
kukosa nidhamu katika matumizi ya fedha.
Tito 3:14 Watu wengi hasa waliokoka,
hawana nidhamu katika matumizi ya fedha pindi inapofika katika mikono yao.
Hawana malengo mazuri katika mtumizi ya fedha na kwa sababu hiyo wanajikuta
fedha wanayoipata inatumika kienyeji na kwa sababu hiyo tatizo la fedha lina
baki palepale.
Tano,Ufahamu
mdogo wa Neno la Mungu kuhusu fedha.
Wakristo wengi sana wanayo mistari mingi sana inayozungumza uponyaji na
kutoa mapepo, na hata imani yao imeongezeka kwenye maeneo hayo. Lakini kwenye
eneo la pesa ufahamu wao ni mdogo sana, si wengi wanaopata mafundisho katika
nyanja ya fedha ya kutosha.
Sita,
Kuwategemea wanadamu na si Mungu .
Katika Yeremia 17:5 Mungu ametoa ole kwa wale wanaowategemea wanadamu.Hii
pia imekuwa sababu kubwa sana ya tatizo la pesa kuwa sugu. Ni kweli watu
wanamuomba Mungu awabariki, lakini mioyo yao inawategemea wanadamu na tayari
ole imeshatiliwa kwa mtu anayemtegemea mwanadamu ki-mafanikio.
Mwisho,
ni vifungo na laana za kifamilia, kiuokoo, kitaifa nk.
Kwenye eneo la pesa, kuna baadhi ya
watu wamefungwa wasifanikiwe kifedha katika ulimwengu wa kiroho. Hili ni tatizo
la kiroho zaidi na pia wengine ni laana zinazotokana na kushindwa kulijua neno
la Mungu. Soma kumbukumbu 28:15-60.
Ni maombi yangu kwamba Mungu akusaidie
kuwa na mahusiano mazuri na yeye hasa kwenye eneo la fedha ili uone baraka
zake.
Na:
Patrick Samson Sanga.