Wednesday, May 2, 2012

Chakula cha Uzima: Uhuru Wako Katika Kumtumikia Mungu, Unategemea Uhusiano Wako Na Mwenzi Wako



Biblia katika kitabu cha Mwanzo 2:18 inasema ‘Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’. Ni kusudi na mpango wa Mungu watu waoe na kuoana. Hii ni kwa sababu kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea ndoa au wanandoa pia. Naam kwa Mungu ni muhimu sana kujua nani anakuwa mwenzi wako wa maisha tegemeana na kusudi lake la kukuumba.


Tunapoenda kufunga mwaka nimesikia ndani kuweka ujumbe huu kwenye blog hii nikiamini utawafaa wengi. Jambo la msingi ambalo nataka ulipate ni kuhusu uhusiano uliopo kati ya ‘uhuru’ wa kumtumikia Mungu na ndoa yako. Pengine si wengi wanaojua umuhimu wa mahusiano mzuri baina yao kama wanandoa na kumtumikia Mungu. Naam ndiyo maana kuna ujumbe huu kwa ajili yako.

Watumishi wengi katika nyakati za leo hawajawapa heshima na nafasi ambayo wenzi wao wanaistahili. Baadhi ya wanaume wameona kupata mke ni sehemu ya kukamilisha sifa za utumishi wao kama wanandoa bila kujua kwa nini ameunganishwa na huyo mwenzi wake. Wengine wamekuwa wakiwapuuza wake au waume zao na bado madhabahuni wanalihubiri neno. 

Na kuna baadhi yao hawana upendo kwa wake zao, wake nao  si watiifu kwa waume zao, ni watu wa kugombana, wenye uchungu ndani yao nk, naam bila kutengeneza au kumaliza tofauti zao hizo  utawakuta madhabahuni wakihudumu kwa raha kabisa. Je, jambo hili ni sahihi kweli? Je ni jambo la kumpendeza Bwana?

Fahamu kwamba ‘uhuru wako katika kumtumikia Mungu kwenye nafasi aliyokupa katika mwili wake, ipo kwa mwenzi wako wa maisha’. Ilikuwa Desemba 28, 2010, Bwana Yesu aliponifundisha jambo hili. Naam uhuru wako wa kumtumikia Mungu upo kwa mke/mume wako. Hivyo kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri huwezi kutumika katika mapenzi yake. Naam uhuru wa wewe kusikia na kupokea kutoka kwa Mungu unategemea sana mahusiano yako na mwenzi wako.

Nilipofuatilia tafsiri ya neno hili uhuru (freedom) niligundua zipo tafsiri nyingi lakini nikachukua hizi tatu kwa kuwa zinaendana na ujumbe huu.  Tafsiri moja wapo ya ‘Oxford dictionary’ inasema uhuru ina maana ya ‘special privilege or right of access’.  Na tafsiri ya neno hilo kutoka katika ‘Encarta dictionary’ ni ‘right to use or occupy a space’ na pia tafsiri nyingine ni ‘ease of movement’.


Naam mahusiano yako na mwenzi wako yanapokwa mazuri jambo hili linakupa haki, kibali, nafasi na mpenyo wa kumtumika Mungu katika kiwango alichokusudia na zaidi katika mapenzi yake. Jambo hili linakupa mpenyo wa kusikia, kuhoji na kusemezana na Mungu juu ya kile ambacho anataka uwafundishe watoto wake ama ukiwa madhabahuni, au kwa njia ya kuandika, kushuhudia nk. Naam kwa hiyo mahusiano mazuri kati yako na mwenzi wako ni ufunguo wa wewe kumtumika Mungu.

Si hivyo tu bali mahusiano yako na mwenza wako yanapokuwa mazuri utapata wepesi wa kutembea na kutumika katika kusudi la Mungu. Naam ndivyo unavyopata haki ya kutumia kila ambacho Mungu ameweka ndani yako kwa utukufu wake, naam ndivyo unavyokuwa na nguvu ya utawala kwenye nafasi na eneo lako la utumishi katika ulimwengu wa roho.

Biblia inasema katika 1Petro 3:7 ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’.
Naamini umeona kile kipengele cha mwisho kinavyosema. Hii ina maana kama mwanaume atashindwa kukaa na mke wake kwa akili na kumpa heshima, maombi yake yatazuiliwa. Sasa fikiri mwanaume huyu ni mtumishi yaani Mchungaji, Mwalimu, Nabii nk nini kitatokea kwa wale anaowachunga au kuwahudumia? Naam mahusiano yako na mwenzi wako ni ya maana sana kama unataka kutumika katika mapenzi ya Mungu. Mahusiano mazuri baina yenu yanaleta mawasiliano mazuri baina yako kama Mtumishi na Mungu wako. Hivyo msingi wa mawasiliano mazuri na Mungu wako, upo kwa mwenzi wako.

Ni vizuri ukafahamu kwamba bila kuwa na mahusinao mazuri na mwenzi wako wa maisha, utumishi wako ni bure. Naam uhuru wako katika kumtumika Mungu unategemea uhusiano wako na mwenzi wako. Si rahisi kwa Mungu kusema na wewe kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri, matokeo yake utawasikizisha/hubiri/fundisha watu mawazo yako na pengine ya adui, zaidi utahudumu kwa mazoea bila uwepo wa Bwana, au chini ya kiwango cha upako uliokusudiwa, tena ni kwa sababu Mungu anawaonea huruma watu wake.

Jifunze kufanya tathimini ya mahusiano yako na mwenzi wako mara kwa mara, na kuhakikisha unayaboresha, naam jambo hili ni muhimu sana kwenu binafsi na zaidi kwa Mungu ili kupata uhuru wa kusikia kutoka kwake kila wakati kwa ajili yenu na  wale ambao amekupa kuwahudumia.

Nakutakia utumishi mwema katika nafasi yako pamoja na mwenzi wako, mwenzi wako ni wa muhimu sana, mpe nafasi yake, utaona mabadiliko kwenye utumishi wako.

Mwl Patric Sanga
0755-816800

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...