Thursday, May 24, 2012

Taifa Stars Stars kuombewa leo Biafra ili icheze Kombe la Dunia


"Katika vingele 14 vya maombi tutakayofanya kesho (leo) tutaiombea timu yetu iishinde Ivory Coast ili ijitengenezee njia nzuri ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Mbona wale Zambia timu ya wachezaji wasiokuwa na majina waliweza kuwafunga kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika na kuchukua ubingwa kwanini sisi tushindwe?'' alihoji Askofu Gadi.

WAUMINI wa madhehebu mbalimbali ya dini ya kikristo leo wanatarajia kukusanyika katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine pia wataiombea Timu ya Taifa (Taifa Stars) ili ifuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014.

Askofu Charles Gadi

Akizungumzia na waandishi wa habari jijini jana wakati akitoa tathimini ya siku 100 za maombi hayo kati ya 900 zilizobaki za kuliombea taifa mambo mbalimbali yakiwemo ya michezo, Mwenyekiti wa Huduma ya Good News For All Ministry Askofu Charles Gadi, alisema kuwa upo Stars ikaishinda Ivory Coast kwa kumtegemea Mungu kwani kwake hakuna lisilowezekana.

"Katika vingele 14 vya maombi tutakayofanya kesho (leo) tutaiombea timu yetu iishinde Ivory Coast ili ijitengenezee njia nzuri ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Mbona wale Zambia timu ya wachezaji wasiokuwa na majina waliweza kuwafunga kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika na kuchukua ubingwa kwanini sisi tushindwe?'' alihoji Askofu Gadi.

"Wale wote (Ivory Coast) ni wachezaji wenye majina makubwa duniani lakini walitolewa na Zambia wasiojulikana, hata sisi tunaweza kuwatoa," alisema.
Chipolopolo iliifunga Ivory Coast kwenye mchezo wa fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Gabon Februari mwaka huu kwa mikwaju ya penalti 8-7 na kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza.

Wakati huohuo, kocha mpya wa timu ya Taifa Stars, Kim Poulsen jana alitimiza wiki moja tangu alipochukua mikoba ya Jan Poulsen na kutoa tathmin ya mwenendo mzima wa programu ya mazoezi.

Timu ya Taifa (Taifa Stars)
Kim alianza kibarua rasmi cha kukinoa kikosi cha Stars Jumatano iliyopita, kijiwinda na mchezo dhidi ya Ivory Coast utakaochezwa Juni 2, mwaka huu, kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil 2014.
"Ni jambo jema kwangu na wachezaji kwa ujumla kuhakikisha kila mmoja wetu anaipenda kazi yake na kujituma kwa ajili ya taifa lake," alisema Kim.

"Binafsi hilo nimeliona kwa siku hizi chache za mazoezi ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Ivory Coast na kuiona kazi yangu kuwa nyepesi kwa kiasi fulani,"
"Kila mmoja wetu ameonyesha nidhamu ya mchezo, nafikiri ni hatua moja ya mafanikio ambayo tumeipiga kwa siku hizi chache za mazoezi."

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...