Je! Unaamini
ya kuwa Mungu anaweza kusema na watu kwa njia ya ndoto? Najua ni rahisi kuamini
kuwa Mungu alisema na watu zamani kwa njia ya ndoto kama tunavyosoma katika
Biblia; lakini je! Unaamini ya kuwa Mungu anasema na watu kwa njia ya ndoto
siku hizi?
Mwl Christopher Mwakasege |
Najua kuna
watu wanaoamini na wengine hawaamini. Sijui wewe uko upande gani.
Lakini
nataka nikueleze hivi; Kufuatana na Biblia kuna ndoto za aina tatu;
(a)
Kuna ndoto kutoka kwa Mungu. Soma kitabu cha Hesabu 12:6, na Yoeli 2:28.
(b)
Kuna ndoto zinakuja kwa sababu ya shughuli nyingi. Soma kitabu cha Mhubiri 5:3.
(c)
Kuna ndoto za uongo zinazotoka kwa shetani aliye baba wa uongo. Soma kitabu cha
Yeremia 23:52 na Yohana 8:44.
Unaweza kutofautisha kwa namna gani tofauti iliyopo kati ya hizi ndoto? Na
utajuaje kuwa ndoto uliyoiota imetoka kwa Mungu? Kila ndoto lazima ipimwe na
Neno la Mungu. Ikiwa imetoka kwa Mungu, ni lazima utakuta neno la Mungu ambalo
linaeleza maana yake. Mara nyingine ndoto toka kwa Mungu huja kama fumbo;
lakini Roho Mtakatifu ajuaye kuyafumbua mafumbo ya Mungu (1 Wakorintho
2:10,11), atalifunua fumbo hilo kwa kukuonyesha neno la Mungu linalofanana na
ndoto hiyo.
Si busara kuzikubali ndoto zote unazoota bila ya kuzipima katika Neno la
Mungu. Na pia si busara kuzikataa ndoto zote bila kuzipima katika Neno la
Mungu.
Nimeona nianze kwa kukueleza haya kwa kuwa chanzo cha kuandika kitabu hiki,
ni ujumbe wa Mungu ulionijia kwa njia ya ndoto.
Ndoto yenyewe ilikuwa hivi: Niliona katika ndoto mtu mmoja mkristo, tena
aliyeokoka akifanya mambo ya zinaa bila hata kuogopa. Na wakati nilipokuwa
nikimtazama na kusikitika, nikasikia sauti toka juu yangu ikisema;
“ NITACHUKULIANA MPAKA LINI NA MWANADAMU AFANYAYE
MAMBO YA JINSI HIYO?” Baada ya
kusikia maneno hayo nikaamka.
Wakati huo ulikuwa ni alfajiri, na ndoto hiyo ilinipa maswali na masononeko
mengi moyoni mwangu. Na niliamua kumshirikisha mke wangu Diana juu ya ndoto
hiyo.
Mke wangu akaniuliza; “ Maana yake nini ndoto hiyo?”
Nilipotaka kufungua kinywa ili nimjibu uchungu mzito ulijaa moyoni mwangu,
nikasikia kuugua rohoni, na mara nikaanza kulia!
Unaweza ukaniuliza; “Mwakasege kwa nini ndoto ikulize machozi?”
Hili ni swali zuri. Hata mimi nilijiuliza kwa nini nitoe machozi kwa ajili
ya ndoto. Lakini baada ya kulifuatilia jambo hili katika maombi na katika neno
la Mungu nilielewa sababu yake.
Je! Unafahamu matokeo ya Mungu kusema “Nitachukuliana mpaka lini na
mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Ukisikia maneno ya jinsi hii ujue
Mungu amekasirika na kuna maangamizo mbele.
Hebu na tulifuatilie jambo hili katika biblia ili tulione uzito wake.
Nuhu na Gharika.
Ni vizuri ukumbuke ya kuwa gharika ilitokea wakati wa Nuhu kwa sababu ya
zinaa.
“Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi
na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliona hao binti za wanadamu –
ni wazuri; WKAJITWALIA WAKE WO WOTE WALIOWACHAGUA. Bwana akasema, ROHO YANGU
HAITASHINDANA NA MWANADAMU MILELE, kwa kuwa yeye ni nyama; basi siku zake
zitakuwa mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile, tena
baada ya hayo, wana wa Mungu WALIPOINGIA kwa binti za wanadamu, wakazaa nao
wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA AKAONA YA
KUWA MAOVU YA MWANADAMU NI MAKUBWA DUNIANI NA KWAMBA KILA KUSUDI ANALOWAZA
MOYONI MWAKE NI BAYA TU SIKU ZOTE.
BWANA AKAGHAIRI KWA KUWA AMEMFANYA MWANADAMU
DUNIANI, AKAHUZUNIKA MOYONI. Bwana akasema, Nitamfutilia usoni pa nchi;
mwanadamu na mnyama, na kitambulisho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya
kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.” (Mwanzo 6:1-8)
Ukiendelea kufuatilia habari hii katika Biblia utaona ya kuwa baada ya
gharika ya maji walibaki watu nane tu! Wanadamu wengine wote waliangamia kwa
sababu ya nini? – Zinaa!
Sodoma
na Gomora
Wasomaji wa Biblia wanafahamu kabisa ya kuwa miji ya Sodoma na Gomora
iliteketezwa kwa moto baada ya Mungu kuihukumu kwa sababu ya uasherati uliokuwa
ukifanyika ndani yake. Soma Mwanzo 19:4-25.
Na pia katika kitabu cha Yuda 1:7 tunasoma hivi: -
“Kama vile Sodoma na Gomara, na miji iliyokuwa kando
kando, waliofuata UASHERATI kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya
mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa
milele.”
Ikiwa Mungu aliwatenda hivi watu wa Sodoma na Gomora, ni kitu gani
kinamfanya mwanadamu wa siku hizi adhani ya kuwa Mungu amebadilika juu ya
kuadhibu wale wote wafanyao uasherati? Katika miji hiyo miwili ni watu watatu
tu waliobaki – Lutu na watoto wake wawili! Wanadamu wengine waliokuwa katika
miji hiyo waliteketezwa kwa sababu ya nini – Zinaa!
Kuhani Eli na watoto wake.
“Basi Eli
alikuwa mzee sana, naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda
Waisraeli; na jinsi WALIVYOLALA NA WANAWAKE waliokuwa wakitumika mlangoni pa
hema ya kukutania.” (1Samweli
2:22)
Hata baada
ya baba yao kuwaonya hawakusikia, na matokeo yake ni:-
1.
Watoto hao wawili, Hofni na Finehasi walikufa wote siku moja;
2.
Wana wa Israeli walipigwa na adui zao Wafilisti na Sanduku la agano likatekwa;
3.
Kuhani Eli alikufa.
Yote haya yalitokea katika taifa ambamo watoto wawili wa kiongozi waliuwa
wakifanya mambo ya Zinaa bila hata kujali maonyo.
Je! Bado unajiuliza kwa nini nilitoa machozi baada ya kusikia sauti ya
Mungu katika ndoto ikisema “Nitachukuliana mpaka lini na mwanadamu afanyaye
mambo ya jinsi hiyo?”
Itaendelea..
Na Mwl C.Mwakasege
Bwana Yesu tusamehe watt wako,tupo kwenye dunia iliyochafuka,sisi ni wa dhambi.tunatubu na kuomba msamaha wa dhambi nyingi mno siwezi kuzitaja.ooh
ReplyDeleteninasikia uchungu pia baada yakusoma, Mungu anirehemu kwa kumkosea kwa njia ya zinaa, tunahitaji kukiri na kutubu ili Mungu atusamehe. Mungu wangu nirehemu....
ReplyDeleteNasikia uchungu mwingi baada ya kusoma na nikumbuka uzinzi mwingi uliombatana nami, ee Mungu wa rehema nyingi utusamee, unirehemu na wasamee wote tulianguka katika zinaa.. Mungu wangu nisamehe, nirehemu na naomba unisaidie maana mawazo yangu yamejaa zinaa...
ReplyDeleteNisamehe Mungu wangu,nimeyajua mimi makosa yangu.usitazame dhambi zangu kwa kiasi cha rehema zako uyafute makosa yangu.
ReplyDeleteEee Mungu nirehemu mimi na niokoe na maana hiyo
ReplyDeleteEee Mungu nirehemu mimi na niokoe na maana hiyo
ReplyDeleteEehhh Jehovah Nisi, Nisamehe Mimi na familia yangu kwa kukutenda dhambi ya zanaa, nakuomba utuongoze kwa mkono wako uliohodari na mtakatifu, uliojaa upendo na mafundisho tukatende yakupendezayo wewe pekee. amina
ReplyDeletenikweli mungu atatumaliza tuzipo tubo
ReplyDelete