Thursday, May 24, 2012

Package From Altar: Siyo busara kusema kwamba "hakuna kuokoka - Askofu Zakaria Kakobe


Hata kama mtu hanywi pombe, havuti sigara au siyo mwizi, bado tu atakwenda katika moto wa milele kutokana na asili ya dhambi iliyomo ndani yake

Siyo busara kusema kwamba "hakuna kuokoka, haiwezekani kuokoka," huku hatujui hata maana ya kuokoka. Mtu mwenye busara kwa mfano, hawezi kusema hakuna ”Nguvu ya Uvutano“ huku hajui hata maana ya nguvu hiyo.
  Watu wengi watajikuta wanakwenda katika mateso ya Jehanam ya moto, kwa sababu tu hawajui maana ya kuokoka, na jinsi ya kuokoka katika mateso hayo. Sasa basi, ni nini maana ya kuokoka?

Askofu Zakaria Kakobe
Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kumpata mtu.Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo, adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri.

Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika; hapo tunasema mtu aliyesalimika au kunusurika, ameokoka. Kwa mfano, mtu asiyejua kuogelea anapotumbukia baharini baada ya mashua aliyokuwa anasafiria kupinduka, halafu akaanza kunywa maji, na kuwa katika hatari ya kufa maji; anapotokea bingwa wa kuogelea, na kumsalimisha mtu wa jinsi hiyo, hapo tunasema kwamba bingwa wa kuogelea, amemuokoa mtu huyo, na mtu huyo ameokolewa au ameokoka.

Miaka kadhaa iliyopita  katika nchi yetu ilitokea ajali mbaya ya meli ”Mv Bukoba.“ Meli hiyo ilizama  katika Ziwa Victoria ikiwa na abiria; na mamia kwa mamia walikufa maji .Meli hiyo ilipinduka na kuzama, ikiwa chini juu. 

Mpaka leo, haikuwezekana kuitoa ile meli majini, na hivyo mamia hao ”walizikwa“ katika meli hiyo. Yalikuwa ni maombolezo makubwa ya kitaifa. Ninamfahamu dada mmoja ambaye alikuja kuniona, ili nimwombee kwa Mungu; apate faraja, na kutoka katika hali ya mawazo mengi. Dada huyu alifiwa na ndugu zake 22, kwa mpigo, na wote walizama  katika meli hiyo, na hakuna hata mmoja aliyepatikana hata mwili tu wa kuzika. Ndugu hawa wote walijikusanya Dar-Es-Salaam, Dodoma, Tabora na Mwanza na kwenda Bukoba kwenye msiba.

Baada ya msiba, wakaamua wote kwa pamoja kurudi kwa meli hiyo, siku hiyohiyo moja. Matokeo yake, ikawa ni  kupata ajali hiyo na kufa maji. Hata hivyo, pamoja na mamia kwa mamia kufa maji katika ajali hiyo mbaya, wako watu wachache ambao walinusurika kufa. Vyombo vya habari vilipokuwa vikitoa taarifa hii, vilisema ”Watu waliookoka katika ajali ya ”Mv Bukoba“, waelezea mkasa uliowapata“. Wale walionusurika katika ajali hiyo, walisemekana wameokoka.

Baada ya kuelewa maana ya neno ”Kuokoka“, hatuna budi kufahamu kwamba, neno ”kuokoka“, linatumika kwa maana hiyohiyo, linapokuwa linahusishwa na ”walokole.“ Labda utaniuliza, ”Kwa vipi walokole wameokoka? Wamenusurika katika mkasa upi?“ Katika kujibu swali hili, unahitajika ufafanuzi wa kina ili tupate kuelewa. Tufuatane sasa hatua kwa hatua, ili upate kuelewa.

Wanadamu wote ni wenye dhambi kutokana na asili yetu. Kutokana na mzazi wetu Adam aliyefanya dhambi, sisi sote tunazaliwa tukiwa na asili ya dhambi na hivyo kujikuta tunatenda dhambi. Kwa mtu mmoja (Adam), dhambi iliingia ulimwenguni na kila mmoja wetu anahesabiwa kuwa na dhambi (Warumi 5:12). Biblia inasema katika Zaburi 51:5, ”Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani.“ Sisi sote, tunazaliwa tukiwa na asili ya dhambi. 

Ndiyo maana utaona mtoto mdogo anasema uongo, ana hasira, wivu n.k. Mtoto mdogo akisikia muziki wa dansi, atakata viuno na kucheza, bila hata kufundishwa. Mtoto mdogo akinyimwa au kucheleweshwa ”nyonyo“ au kunyonya ziwa la mamaye, atakasirika na kumpiga mamaye kofi pamoja na kamkono kake kadogo. Hasira hii imetoka wapi? Ni kutokana na dhambi ya asili ya Adam.

Hivyo kutokana na asili ya dhambi, kila mtu anahesabiwa kuwa ni mwenye dhambi; awe anavuta sigara au havuti sigara. Awe anakunywa pombe au hanywi pombe. Awe anafanya uasherati  au hafanyi uasherati. Awe anafanya dhambi hii au nyingineyo, bado kila mwanadamu ni mwenye dhambi. Awe anafanya dhambi nyingi au chache, hiyo haijalishi, bado mwanadamu ni mwenye dhambi kutokana na asili yake. Mnazi unabaki mnazi, ukitoa nazi elfu moja, nazi kumi au usipotoa nazi kabisa. 

Mnazi, ni mnazi, kutokana na asili yake ya mti.  Mwanadamu yeyote, hata akijitahidi kutenda mema, ni kazi bure, bado mbele za Mungu, anahesabiwa kuwa hana haki, ni mkosaji, kutokana na asili yake ya dhambi.Tunasoma katika AYUBU 9:29-31, Nitahukumiwa kuwa ni mkosa; Ya nini nitaabike bure?  Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji,na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni; lakini utanitupa shimoni.“  Tena tunasoma katika ISAYA 64:6, ”Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi.“
Sasa basi, matokeo ya dhambi ni nini? Ni adhabu. 

Hakuna mwenye dhambi atakayekosa adhabu. Lazima kila mwenye dhambi atapata adhabu ya milele yaani kutupwa katika ziwa la moto na kutengwa na Mungu milele (WARUMI 6:23; UFUNUO21:8). Hakuna mtu yeyote mwenye dhambi, yaani asiyekuwa na haki mbele za Mungu atakayeokoka katika adhabu hiyo. Biblia inasema katika ZABURI 119:155, ”Wokovu u mbali na wasio haki“. 

Kutoa sadaka nyingi, kusali mara tatu au mara tano kwa siku, kuimba kwaya, kipaimara, ubatizo wa utotoni au tendo lolote linaloonekana jema kidini, haliwezi kumfanya mtu anusurike katika adhabu hii ya moto wa milele. Hata kama mtu hanywi pombe, havuti sigara au siyo mwizi, bado tu atakwenda katika moto wa milele kutokana na asili ya dhambi iliyomo ndani yake. Dhambi ya asili ya Adamu, inatosha kabisa kumtupa mtu katika moto wa milele bila nyongeza yoyote ya dhambi.

Itaendelea Alhamis Ijayo

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...