Utangulizi
Mkristo ni nani?
Mkristo ni mtu aliyemwamini Yesu Kristo na kumpokea au kumfanya Bwana na Mwokozi wa maisha yake (Warumi 10:9-10). Haitoshi tu kusema, ‘Mkristo ni mtu aliyemwamini Yesu’, kwasababu Biblia inasema ‘hata shetani naye anaamini na kutetemeka pia’ lakini si mkristo (Yakobo 2:19)
Uchumi ni nini?
Uchumi ni Maarifa ya namna ya kutumia rasilimali (resources) zilizopo au chache (scarce) ili kukutana na mahitaji na matakwa mengi (needs and wants) katika maisha ya mtu/watu.
Ni mapenzi ya Mungu tuyafurahie maisha yetu aliyotupa yeyé hapa duniani kama anavyosema katika kiyabu cha Isaya 1:19 ‘mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi.’ Na kila kitu unachohitaji kwa ajili ya maisha mazuri ya utoshelevu, kipo hapa hapa ulipo.
|
Mwl. Mgisa Mtebe |
Rasilimali zote tunazozihitaji kwa ajili ya Maisha mazuri ya Baraka, tunazo hapa hapa. Lakini wewe kama Mkristo, hautaweza kuyafurahia maisha aliyokuandikia Mungu, uyaishi hapa duniani, kama hutajua namna/jinsi/mbinu/kanuni za ki-Mungu za kufanikiwa kimaisha ili kukutana na mahitaji yako na matakwa yako ya kimaisha.
Tujifunza siri na kanuni za kufanikiwa kiuchumi kwa maisha ya tajiri mmoja, aliyeandikwa katika Biblia, na jinsi alivyofanikiwa sana kimaisha na kiuchumi, japo alianza maisha kwa shida na taabu. Mtu huyu tajiri anaitwa Yakobo. Habari hii utaipata katika kitabu cha Mwanzo 28:1-5; 29: 13-30; 30:25-43; 31:1-3; 32:1-18
Kwa ufupi ni kwamba:
Yakobo alipomkimbia ndugu yake Esau, alifika kwa mjomba Labani akiwa na fimbo tu, lakini baada ya kukaa huko kwa muda, alirudi katika nchi ya Baba zake akiwa tajiri mkubwa mwenye wafanyakazi 1,200 (Matuo mawili = Makundi mawili ya watu 600) Soma Mwanzo 32:9-12. Fikiri mwenyewe, mtu mwenye wafanyakazi 1,200 alikuwa ana wanyama wangapi? Thamanisha mali zake kwa fedha ya sasa.
Utakapokwenda kuisoma habari hii, utaona jinsi Yakobo alivyokuwa tajiri, kwa maana alikuwa na uwezo wa kutoa zawadi kwa mtu, kiasi cha punda 200, farasi 200, ngamia 200, ng’ombe 200, kondoo 200 na mbuzi 200. Utajiri huu kwa lugha ya sasa; Punda 200 (kiuchumi, hii inakadiriwa kuwa ni sawa na magari madogo ya mizigo (pickup) 16; yaani punda 12 wanaweza kubeba mzigo wa pickup 1). Kondoo 200 ni sawa na maduka 4 ya nguo, ngamia 200 ni sawa na malori madogo ya mizigo 16, farasi 200 ni sawa na pikipiki 50.
Unaweza kuona jinsi Yakobo wa Isaka alivyokuwa tajiri. Mtu anayeweza kukupa zawadi ya pikipiki 50, maduka 4 ya nguo, malori madogo 16 na magari madogo ya mizigo (pickup) 16; yeyé anabakiwa na kiasi gani cha utajiri? Na kama alianza akiwa mikono mitupu, alitumia njia gani kufikia katika mafanikio hayo ya kiuchumi? Hata mimi nataka kujua. Utashangaa kwamba, Biblia inafundisha uchumi kiasi hiki.
KANUNI ZA KIBIBLIA ZA UCHUMI MZURI
Maono - Kuona Fursa za kiuchumi
Mafanikio hayaji kwa bahati mbaya au nzuri, bali yanapangwa. Ukiona mtu amefanikiwa kiuchumi, ujue aliona kwanza fursa hiyo na akaichuchumilia na kuifuatilia mpaka akafanikiwa. Hivyo muombe Mungu akupe kuziona fursa zilizopo. Tafuta kuona mahitaji mbalimbali ya jamii, huwezi kukosa kuona fursa kadhaa za kiuchumi.
Utakapokwenda kusoma habari hizi, utagundua kwamba, mjomba Labani alikuwa tajiri mwenye shughuli mbalimbali na wafanyakazi wengi sana. Kwa muda mfupi ambao Yakobo alikaa kwa mjomba wake, aligundua kwamba, ataweza kufanikiwa kwa kujishughulisha na kazi mojawapo za mjomba, hivyo akachagua kujikita katika mifugo ya mjomba Labani. Mwanzo 29: 15-20.
Mafanikio hayaji kwa bahati mbaya au nzuri, bali yanapangwa. Lazima uwe na uwezo wa kuona fursa za kiuchumi na kujitosa humo baada ya kufanya upembuzi yakinifu. Ukiona mtu amefanikiwa kiuchumi, ujue aliona kwanza fursa hiyo na akaichuchumilia na kuifuatilia mpaka akafanikiwa. Soma Mwanzo 21:14-19 na Waefeso 1:15-19 utaona umuhimu wa kuwa na macho yanayoweza kuona vitu vilivyojificha. Hivyo muombe Mungu akupe kuziona fursa zilizopo. Tafuta kuona mahitaji mbalimbali ya jamii, huwezi kukosa kuona fursa kadhaa za kiuchumi.
Malengo mahususi – Kujua kwa hakika unataka kufika wapi
Alijua alichokuwa anataka na alikaza uso kutoyumbishwa mapaka apate anachotaka. Hii ni tabia ya kila mjasiliamali aliyefanikiwa. Lazima uwe ‘focused’ usiyumbishwe. Utaiona tabia hii ya Yakobo kwa jinsi alivyojaribiwa katika swala la kupata mke aliyemtaka. Alijua anataka mke, na sio bora mke.
Mjomba Labani alikuwa na mabinti wawili, Lea na Raheli. Aliambiwa kama anataka kumuoa Raheli, atoe mahari ya kufanya kazi kwa miaka 7. Baada ya maiaka 7 akapewa Lea badala ya Raheli. Kwa lugha rahisi, alitapeliwa au alizulumiwa. Akaambiwa, kama vado anamtaka Raheli, afanye kazi tena kwa miaka 7 ndipo atapewa Raheli.
Kama Yakobo angekuwa anataka bora mke, angeridhika na Lea, lakini kwakuwa alikuwa anamtaka Rachel, akalenga ‘kutokupumzika’ mpaka ampate Raheli, bila kuyumbishwa. Akaapinda mgongo tena kwa miaka 7 ili tu kuyafikia malengo yake, na akampata mke aliyemtaaka, Raheli !!! Mwa 29:16-18.
Ni muhimu sana kwa mtu kuwa na makusudio ya moyo (Malengo).
Malengo hufungulia nguvu za Mungu (Msaada wa Mungu)
‘Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; na mwanga utaziangazia njia zako’ (Ayubu 22:28)
Malengo hukupa nidhamu ya kimaisha (Descipline)
‘Pasipo maono, watu huacha kujizuia (yaani hukosa nidhamu, au msimamo - huyumba-yumba) (Mith 29:18).
Yeremia 1:5-10; Mungu alimtenga Yeremia kuwa Nabii tangu tumboni mwa mamaye, Je wewe ulitengwa uwe nani? Tafuta kujua mpango wa Mungu kwako. Usipopatia wito wako, kuna hatari ya kutofanikiwa katika baadhi ya vitu unavyohangaika kuvifaya. Mungu anabariki kazi zake, si kila kazi. Ni muhimu uutafuta uso wa Mungu ili ujue mpango wa Mungu juu ya maisha yako. Yeremia 29:11-13, Zaburi 32:8
Mipango Mizuri – Kuwa na njia za kukufikisha katika malengo yako
Mwanzo 30:25-36; Ili kufikia mafanikio na maisha mazuri, mtu wa Mungu si tu kwamba anahitaji kuwa na maono na malengo tu, bali pia anahitaji kuwa na mipango mizuri ya kumfikisha katika maono na malengo yake. Jiulize, ni kwa njia gani nitaweza kufikia kule ninakotamani kufika? Hizo njia utakazopata, ndio tunaita mipango.
Katika habari hii ya Yakobo, unaona anapanga kuwachukua wanyama wa mjomba na kwenda nao umbali wa siku tatu (3) na kukita kambi ya mifugo huko. Na utaona anapanga kukaa huko kwa miaka mitatu (3). Hizi namba unazoziona hapa, ni mipango madhubuti. N mawazo ya mtu aliyefanya uchunguzi wa eneo zuri la kuweka kambi ya mifugo na ni mawazo ya mtu aliyepiga mahesabu kuona, ni baada ya muda gani atakuwa ameweza kutengeneza faida.
Mipango mizuri itazaa matokeo mazuri. Mipango mibaya itazaa matokeo mabaya. Kwahiyo, tafuta namna ya kutengeneza mipango mizuri, ikibidi tumia wataalam wa mipango. Fanya Fisibility study na tengeneza a good Business Plan. Yakobo alijitenga mwendo wa siku 3 na akakaa nyikani muda wa miaka mitatu. Huu ni Mpango wa Shughuli (This is a business plan au activity plan). Baada ya miaka kadhaa, Yakobo alikuwa mtu mwenye mafanikio na utajiri mkubwa, leo tungemuita ‘Milionea’ mkubwa. Kumbuka; Mipango mizuri itazaa matokeo mazuri. Mipango mibaya itazaa matokeo mabaya.
Itaendelea toleo líjalo
Mwl. Mgisa Mtebe,
P. O. Box 837, Dar es Salaam.
Simu: (+255) 0713497654.