Zoezi la kuchimbua dhahabu
inayodaiwa imefukiwa ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli (KKKT), Dayosisi
ya Kusini Usharika wa Brandt wilayani Mbarali mkoani Mbeya, hatimaye
limesitishwa kufuatia kutokea vurugu za wananchi na kuhatarisha amani hali
iliyopelekea polisi kuingilia kati ili kuepusha ghasia zaidi.
Kusitishwa kwa zoezi hilo
kuliamuliwa jana na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele na
imeelezwa kuwa shughuli hiyo itaweza kuendelea ama kutokuendelea kadri
uongozi wa kanisa hilo utakapojadili yaliyojiri katika zoezi hilo.
Mchungaji wa Kanisa la KKKT Usharika
wa Brandt, Emanuel Lunda, akizungumza na NIPASHE iliyofika katika kanisa hilo
lililopo kijiji cha Ihahi, alisema uchimbaji wa madini hayo
uliokuwa ukifanywa ndani ya kanisa hilo karibu na madhabahu ulilenga kutafuta
dhahabu ambazo kama zingepatikana zingeuzwa na fedha zingetumika kujenga
kanisa jipya la kisasa.
Alisema kabla ya vurugu hizo kutokea
na kutolewa amri ya kusitishwa kwa zoezi la uchimbaji, tayari walikuwa
wamechimba urefu wa zaidi ya futi 10, lakini hakuna dhahabu iliyokuwa
imepatikana.
Mchungaji Lunda alisema pia fedha
hizo ambazo zingetokana na mauzo ya dhahabu, zingetumika kujenga nyumba ya
mchungaji na ya Mwinjilisiti wa mtaa wa kanisa hilo pamoja na kuweka huduma ya umeme katka
kanisa jipya ambalo lingejengwa kwa gharama ya Sh. milioni 40 ambayo ilikuwa
imetathiminiwa.
Alisema tetesi za kuwepo dhahabu
ndani ya kanisa hilo lililojengwa miaka ya 1905 na Wajerumani, kwa muda mrefu
zilikuwa zikienezwa na baadhi ya wakazi wa kjijiji cha Ihahi ambapo Mkuu wa
Jimbo la Chimala, Laulent Ng’umbi naye alidokezwa suala hilo ambaye naye
aliwaeleza viongozi wa Dayosisi ya Kusini na hivyo ikaamuliwa ufanyike utafiti
wa madini hayo kwa kuchimba ndani ya kanisa.
Alisema mwanzoni mwa Aprili mwaka
huu uongozi wa Dayosisi, Jimbo na Usharika baada ya majadiliano ya suala hilo,
waliitwa wataalam wa madini ambao walipima ndani ya kanisa kwa kutumia vifaa
maalum vya kutafuta madini ambao walipima mara tatu kwa nyakati tofauti na
kugundua kulikuwa na madini ndani ya kanisa hilo.
Mchungaji Lunda alisema mara ya tatu
wataalam hao walipofika katika kanisa hilo
kwa ajili ya kupima madini hayo waliambatana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya
Kusini, Mwamisole, Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulenti Ng’umbi, Mchungaji
Mbilinyi wa Jimbo la Chunya na Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mchungaji
Mbedule.
“Ilipofika Aprili 18 niliitwa makao
makuu ya Dayosisi Njombe ambapo Askofu Mengele wa Dayosisi ya Kusini,
alinieleza kuwa suala la kuwepo dhahabu ndani kanisa la KKKT Usharika wa Brandt
limejadiliwa kwenye mkutano mkuu wa Dayosisi na kwamba hakuna jinsi ni lazima utafiti
ufanyike,” alisema Mchungaji Lunda.
Aliongeza kuwa kabla ya zoezi la
kuchimba dhahabu ndani ya kanisa kuanza, kuliitishwa kikao cha wazee wa kanisa
na viongozi ambacho kilihudhuliwa na wajumbe 14 wakiwemo wazee wa kanisa,
wajumbe kutoka kamati ya majengo, idara ya vijana, idara ya wanawake na wazee
maarufu wa kijiji cha Ihahi.
Alisema wajumbe wa kikao hicho
walipendekeza kuwa wakati wa zoezi la kuchimba dhahabu ndani ya kanisa kuwe na
usimamizi wa viongozi na waumini ili kusitokee ujanja wa kuibiwa madini na pia
madini yatakayopatikana yauzwe na fedha zitakazopatikana zitumike kujenga
kanisa jipya la kisasa, nyumba ya mchungaji, nyumba ya mwinjilisti na kuweka
huduma ya umeme.
Mchungaji Lunda alisema siku ya
Jumatatu Aprili 23, wachimbaji madini waliokuwa wametafutwa na kanisa walianza
kazi kwa usimamizi wa karibu na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Mwamisole, Mkuu wa
Jimbo la Chimala, Ng’umbi Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mbedule Mchungaji wa
Usharika wa Brandt (Lunda) na Mwinjilisti wa Mtaa, Martin Msigwa.
Alisema zoezi la kuchimba dhahabu
lilianza kati ya majira ya saa 7:00 na saa 8:00 mchana ambapo makubaliano
ilikuwa kazi hiyo iwe inafanyika hadi nyakati za usiku, ilipofika siku ya
Jumanne saa 12:00 jioni alikifika Mwenyekiti wa Kijiji cha Isitu aliyefahamika
kwa jina la Mama Mkwembe ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Ihahi alianza kuhoji
ni kwanini kanisa linachimbuliwa.
“Huyu Mwenyekiti wa kijiji cha Isitu
alipokuja alianza kufoka na kueleza kuwa ninyi mna uroho wa utajiri na kutishia
kutoa taarifa polisi lakini hakuna aliyemjibu kwasababu tulijua suala hili
limefuata taratibu zote na kuruhusiwa na viongozi wa kanisa,” alisema Mchungaji
Lunda.
Aliongeza kuwa baadaye Diwani wa
kata ya Ihahi, Mtendaji wa kata ya Ihahi na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihahi nao
walifika katika kanisa hilo lakini walipopewa
maelezo ya jinsi zoezi hilo linavyoendeshwa
walilidhika na kukubali kuwa liendelee sababu limefuata taratibu zote za kanisa
hilo.
Mchungaji Lunda alisema siku hiyo ya
Jumanne majira ya saa 6:30 usiku Mwenyekiti wa Kijiji cha Isitu akiwa na
askari mmoja aliyetajwa kwa jina la Allen Mwamaja walifika katika kanisa hilo
na askari huyo alianza kufoka kutokana na zoezi hilo na kisha kumnyang’anya
simu ya mkononi na kuondoka nayo.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo,
ilipofika saa 8:00 usiku walifika askari wengine zaidi ambao waliingia ndani ya
kanisa hilo na
kuchukua kamera ya video, kamera ya kawaida, sururu, beleshi (sepetu), tochi,
redio na viatu vya mmoja wa wachimbaji na kuondoka navyo hadi kwa Mkuu wa Kituo
cha Polisi Chimala.
Mchungaji Lunda alisema kutokana na
vurugu hizo, Askofu Mengele wa Dayosisi ya Kusini, alitoa amri zoezi hilo lisitishwe na shimo
lifukiwe kazi ambayo tayari imekwishatekelezwa.
Hii ni mara ya kwanza kanisa
kuchimbuliwa kusaka dhahabu inayodaiwa kufukiwa ndani yake. Ingawa maeneo
mbalimbali nchini kwa sasa yanadaiwa kuwa na dhahabu hakuna kokote ambako
inadaiwa kuwa yamefukiwa na mtu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment