Mchungaji Edward Amri |
Mchungaji Edward Amri wa huduma ya Amri Kuu za Mungu
(AKUZAMU) amewapiga marufuku waumini wake kuacha kuilaumu Serikali kwani
haisaidii chochote katika maisha yao na kufanya hivyo ni kinyume na Neno la
Mungu.
Akifundisha Neno la
Mungu katika ibada kanisani hapo alisema ifikie mahali Watanzania wajiulize nini
wataifanyia nchi yao, kwani sisi kama Kanisa lazima tuwe Baraka kwa Taifa na
siyo kugeuka wapinzania kwa kuilaumu serikali; kinachotakiwa kila Kanisa liwe
na utaratibu wa kuwasaidia waumini wake kwa kuwapa mafundisho ya namna ya
kujikwamua kiuchumi, likiwepo suala la kuwahamasisha waweze kujiajiri ili
waweze kuisaidia serikali katika kutoa ajira na kulipa kodi kwa usashihi.
“Kazi ya Kanisa ni kuisaidia serikali na siyo kuipinga
na kuwatengeneza watu wake yaani waumini kuwa raia wema wenye kuipenda nchi yao
likiwepo suala la kuwakwamua watu kiuchumi kwa kuwafundisha mafundisho sahihi
ya uchumi katika ufalme wa Mungu, kama ambavyo kanisa letu linafanya ambapo
muda si mrefu sisi tutakuwa Baraka katika Taifa kwani waumini wetu wengi
wataajiri na watakuwa na walipakodi wazuri katika nchi yetu”.
Akiongea kwa kujiamini alisema kwa sasa uchumi wa
dunia nzima umekwama na sababu yake ni kwamba ni vigumu sana uchumi wa mfumo
huu kufaulu kwa sababu hauna mbadala, yaani ziada kwani masomo hayo ya uchumi
yanayofundishwa shuleni miaka 20 iliyopita ndio hayo hayo yanafundishwa hivyo
wachumi wetu hawawezi kuwa na la ziada zaidi ya kujifunza masomo ambayo wenzao
waliyagundua zamani na ndio maana hadi hivi sasa hawawezi kutoa majibu ya kuboresha
maisha ya wananchi.
Akitoa mfano alisema kwa sasa nchini kwetu hatuna vitu
ambavyo tumegundua. Kwa mfumo wa uchumi wa kwenye makaratasi hauwezi kutoa
majibu kwani hata hao wachumi endapo masomo yangekuwa na hatimiliki nadhani
sisi tusingekuwa na kitu kwani masomo hayo tunakopi kutoka kwa wenzetu ambapo
hatuwezi kuwa na mbadala na ndio maana unaweza kukuta tunao wasomi wengi wa
uchumi wasipoajiriwa hawawezi kuishi wanachanganyikiwa maana hawana mbadala
Akieleza mikakati ya Kanisa lake amesema wao wameamua
kuisaidia serikali badala ya kuilaumu kwa kuwaelimisha waumini wao masuala ya
uchumi katika ufalme wa Mungu kwa kutumia Neno la Mungu, pamoja na
kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kujiajiri ili waweze kuwaajiri wengine.
Rev Edward Amri akiwa na mkewe mama Susanne |
Akijitolea mfano yeye alisema kabla hajaanza
kumtumikia Mungu alijiajiri kwa kufungua biashara ambapo miaka hivi sasa anao
wafanyakazi wasiopungua mia moja wanaofanyakazi katika biashara zake hivyo
amekua msaada kwa serikali kwa kuipunguzia kero ya ajira kwani ameajiri na
analipa kodi serikalini hivyo amekua Baraka kwa nchi.
Mbali na hilo amekuwa na mkakati wa kuwahamasisha wale
aliowaajiri kutojisahahu badala yake nao wafungue biashara zao nao waweze
kuajiri watu wengine kwani ifikie hatua tuipunguzie mzigo serikali badala ya
kuilaumu.
Amekemea tabia ya baadhi ya watumishi pamoja na
waumini kuilaumu serikali kwa kusema eti inasababisha hali ngumu jambo ambalo
amesema si kweli kwani mazingira ya sasa karibu nchi zote zimekwama ni wakati
wa Kanisa kuisaidia serikali kwa kuwafundisha waumini Neno la Mungu kwa usahihi
pamoja na kuwasaidia kujiajiri badala ya kutumia muda mwingi kuilaumu serikali
jambo ambalo si sahihi.
Tangu mwaka 2012 Kanisa la Akuzamu chini ya kiongozi wake Mchungaji Edward
Amri limeanzisha kampeni kabambe kuisaidia serikali kwa kuiombea pamoja na
kuwahamasisha waumini wake kujiajiri na kuwaajiri wale ambao bado hawana ajira
ambapo pia limekuwa likitoa mafundisho ya uchumi kila siku katika ukumbi wa IPS
Jijini Dar es salaam na kila mwezi, ambapo mwezi ujao linatarajia kuendesha
semina kubwa itakayofanyika katika ukumbi wa Nadd’s ulioko salender bridge
jijini Dar es salaam tarehe ishirini na tano mwezi ujao ambapo wengi wamekuwa
wakihudhuria na mara baada ya mafundisho wengi wamebadilika katika ufahamu wao
na wameanza kuchukua hatua ya kujiajiri.
No comments:
Post a Comment