Wednesday, April 18, 2012

Yesu Kristo Aliomba Umoja Kwa Ajili Ya Nani?-Mwl C.Mwakasege


Mwl C Mwakasege
Neno Umoja maana yake nini?
Yesu Kristo alipokuwa anaomba juu ya Umoja kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yohana sura ya kumi na Saba, alilitumia neno Umoja mara tano.
Neno Umoja linaweza kuwa na maana mbali mbali, kutokana hasa na mtu anayelitumia, mahali anapolitumia na kwa ajili ya kitu gani.

Neno Umoja likitumika kwa ajili ya watu lina maana ya patana, afikiana, elewana na lingana, katika roho, na nia, mawazo, maneno  na matendo.
Yesu Kristo alipokuwa akitumia neno Umoja, alikuwa anamaanisha hao anaowaombea wapatane, waafikiane, waelewane, na walingane katika roho zao, nia zao, mawazo yao, maneno na matendo yao.

Sasa, hili si jambo dogo! Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani, akiwa amevaa mwili wa kibinadamu; kabla ya kufa na kufufuka; aliomba maombi ya namna nyingi. Na mojawapo ya maombi yake kwa Baba Mungu, yalikuwa juu ya Umoja wetu.
“Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na Umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. 

Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao; nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi (Yohana 17:20 – 23).Haya ni maombi yaliyowekwa mikononi mwa Mungu, kwa uzito wa kipekee. Yesu Kristo alipokuwa anaomba maombi haya, alikuwa anajua anaongea na nani, na umuhimu wake ni nini.

Yesu alikuwa anamuombea nani?

Tusipoelewa Yesu Kristo alikuwa anaomba umoja kwa ajili ya nani, hatutaweza kufahamu kwa undani sababu zilizomfanya aombe kwa namna hiyo na kwa wakati huo. Ukizunguka katika vikundi mbali mbali vya watu wa Mungu, utakuta wanasema tuombee umoja. Hili ni jambo muhimu sana, lakini si wote ambao wanafahamu ya kuwa maombi yao ni tofauti na yana lengo lisilofanana na sala ya Bwana Yesu.

Inawezekana hata wewe, umewahi kuomba juu ya umoja. Je huwa unaomba umoja wa watu gani? Au huwa unaomba juu ya umoja wa watu wote? Au huwa unaomba umoja wa madhehebu? Watu wengi sana wanapoomba juu ya umoja, kwa kusimamia maombi ya Bwana Yesu, huwa wanaomba juu ya umoja wa madhehebu yao.

Lakini nataka ujue, ya kuwa Yesu Kristo alipokuwa anaomba umoja, katika mistari tuliyosoma, alikuwa haombi juu ya umoja wa madhehebu, wala alikuwa haombi juu ya umoja wa watu wote wa ulimwengu. Yesu alikuwa na mawazo tofauti kwa ajili ya maombi yake.

Narudia tena swali hili; Yesu Kristo alipokuwa anaomba juu ya umoja, alikuwa anaomba kwa ajili ya nani? Kwa sababu Yesu Kristo alifufuka, na yuko hai hata sasa na hata milele, naona ni vizuri tumuulize yeye mwenyewe swali hili.

Je, Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, ulipokuwa unaomba juu ya umoja, ulikuwa unamuombea nani? Tunakuomba tunapolisoma neno lako, Roho wako Mtakatifu atutie nuru katika macho yetu ya kiroho, tupate kuelewa na maandiko.
Yesu Kristo ni Neno (Yohana 1:1-5,14). Kwa hiyo tunapolisoma Neno; tunamsoma Kristo na mawazo yake. Na kwa ajili hiyo, tunapata jibu la swali tulilomuuliza Bwana, kwa kulisoma Neno la Mungu, ambalo ndilo lililobeba mawazo yake.
Yesu aliomba Umoja kwa ajili ya Kanisa.

Napenda kukiri wazi ya kuwa, neno kanisa bado halijaeleweka vizuri kwa watu wengi. Kwa hiyo ninaposema ya kuwa, Yesu aliomba Umoja kwa ajili ya kanisa, nina maana ya kulitumia neno kanisa kama vile linavyotumika na Biblia.
Kanisa maana yake nini?Kuna mtu mmoja ambaye aliniuliza maswali mbali mbali juu ya mapokeo ya madhehebu ya kikristo, na kwa nini mengi ya mapokeo hayo yanapingana.Na mimi kabla ya kumjibu nilimuuliza swali hili; “Je, unafahamu tofauti iliyopo katika dhehebu na kanisa? Akasema ‘ndiyo’.Nikamuuliza tena; ‘Kanisa ni kitu gani’ Akasema; ‘Kanisa ni jengo ambalo tunakwenda kila Jumapili kusali ndani yake’.

Emmanuel Mgaya(Masanja) akiwa katika Semina ya mwakasege Jangwani
Niliposikia jibu hilo, nilipata mshangao mkubwa sana. Nilipata mshangao si kwa sababu jibu lilikuwa ni sahihi. Hapana! Bali kwa sababu jibu hili lilikuwa si sawa. Na zaidi ya hapo limesemwa na mkristo ambaye nilikuwa naamini anafahamu siku nyingi maana ya Kanisa.
Na ndipo nilipoona umuhimu wa mafundisho kwa wakristo. Ni kweli kabisa watu wa Mungu tunahitaji mafundisho yenye uzima na ya kiroho.Sijui huyo Ndugu anaposikia watu wakisema tuombe juu ya umoja wa kanisa, alikuwa anaelewa kitu gani!

Je unafikiri Yesu Kristo alikuwa anaomba juu ya umoja wa kanisa lililojengwa kwa mikono ya wanadamu?
Je! Unadhani Yesu Kristo alikuwa anaomba juu ya umoja wa matofali, vyuma, mchanga, mabati, misumari na saruji?

La hasha! Yesu Kristo alipoomba juu ya umoja, alikuwa haombi juu ya umoja wa jengo tunalokwenda kuabudu ndani yake kila Jumapili au Jumamosi!Kwa nini? Kwa sababu, tunaelewa ya kuwa tunapaswa kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Imeandikwa hivi:“Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”. (Yohana 4:23, 24)Kwa hiyo, kuwa na jengo la kwenda kuabudu kila Jumapili au Jumamosi haitoshi, kama watu wanaoabudu ndani yake hawatamwabudu Baba katika roho na kweli.

Na tena, ni budi tufahamu ya kuwa Mungu ambaye ni Roho, hakai katika majengo yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu (Matendo ya Mitume 7:47-49; Isaya 66:1)Mungu ambaye ni Roho, huishi katika jengo ambalo amelijenga mwenyewe kwa mkono wake, tangu Bwana Yesu alipokufa na kufufuka. Na jengo hilo linaitwa kanisa.

Sasa, kanisa ni kitu gani?

Kanisa ni mwili wa Kristo! Na jambo hili limewekwa wazi katika sala hii ya mtume Paulo:
“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo na utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo, na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo.
kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake, aliutenda katika Kristo alipomfufua katika watu, akamweka mkono wake wa kiume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya KANISA; ambalo ndilo MWILI WAKE” (Waefeso 1:17-23)

Maneno hayo yanatupa picha na maana nzuri juu ya kanisa, ya kwamba kanisa ni mwili wa Kristo. Na kwamba huo mwili ndio ukamilifu wake Kristo, anayekamilika kwa vyote katika vyote. Maneno hayo pia yanaondoa mawazo ya watu wengi wanaofikiri ya kwamba kanisa ni dhehebu fulani au dhehebu lao ndilo kanisa.

Itaendelea....
Na Mwl C Mwakasege


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...